Kufungamanisha Sekta ya Viwanda na Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa Spika, adhma ya nchi yetu kuwa ya Viwanda ni
adhma yetu sote. Jambo hili ni jambo la Maendeleo na halina ushabiki wa
kivyama. Tumepitisha Mpango wa Maendeleo katika Bunge hili na kwa hiyo
ni Mpango wa Nchi sio mpango wa vyama tena. Hivyo sote kwa pamoja
tunafanya kazi ya kuhakikisha tunafikia malengo. Sisi tulio kwenye
upinzani jicho letu pamoja na kushauri na kupendekeza ni kukosoa pale
ambapo walio kwenye Serikali wanakosea. Kukosoa ni tendo la kizalendo na
walio Serikalini wawe tayari kukubali kukosolewa ili kuboresha zaidi.
Kwa maoni yangu, kama tusipofanya marekebisho ya kimkakati mapinduzi ya
Viwanda itakuwa ni nyimbo na ngonjera za kisiasa. Watakaoumia ni
Wananchi ambao hawatapata ajira na Serikali yenyewe itakosa kodi kuweza
kutoa huduma kwa wananchi. Kama nilivyosema hapo awali Serikali
inahitaji kufanya uratibu ili kufikia malengo. Sekta ya Viwanda au
Maendeleo ya Viwanda yanapaswa kufungamanishwa na sekta nyengine za
uchumi kwa sababu kuna kutegemeana. Kwa Tanzania unahitaji Sekta ya
Kilimo inayokua kwa kasi ili kuzalisha malighafi kwenye viwanda. Sekta
nyingine kama Elimu, Afya, Nishati, Mazingira nk zinahusiana na Viwanda
pia. Kwa leo tutazame Sekta Kilimo na Viwanda kwa muktadha wa Hotuba ya
Waziri wa Viwanda na kulinganisha na Hotuba ya Waziri wa Kilimo.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda na Sekta ya Kilimo kwa
pamoja zinachangia nusu ya Pato la Taifa ( GDP) na nusu nyingine ni
sekta ya Huduma. Nadharia za Uchumi zinatuambia kuwa Tija ikiongezeka
kwenye ya Kilimo inawezesha sekta ya Viwanda kukua na kisha sekta ya
Huduma. Hapa Tanzania nan chi nyengine nyingi za Afrika, sekta ya huduma
iliruka hatua hizi na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa sana kwenye
Pato la Taifa. Ndio maana tuna kitandawili nchini kwetu kuwa Uchumi
unakua lakini umasikini haupungui; ni kwa sababu sekta ya huduma haijiri
watu wengi kama sekta ya Kilimo na hivyo uchumi unaokuzwa na sekta ya
huduma ni nadra kuondoa umasikini. Tanzania bado inapambana na
umasikini. Juhudi zote tunazofanya lengo lake ni kuondoa umasikini kwa
watu wetu. Sekta za kuondoa umasikini ni Kilimo na Viwanda hivyo lazima
mikakati ya Serikali iendane na kufungamanisha haya. Ndio Maana Nchi
nyengine Wizara ya Kilimo hujumuisha uongezaji thamani ( Ministry of
Agriculture and Agro-processing ). Hatuhitaji kufanya hivyo,
tunachohitaji ni kufungamanisha. Hata hivyo Serikali imeshindwa kufanya
hivyo katika mwaka wake wa kwanza tu wa Bajeti. Nitaeleza kwa kutumia
changamoto tuliyonayo kuhusu Sukari, Mafuta ya Kula na Nguo.
Mheshimiwa Spika, Malengo ya Serikali kwenye Viwanda yapo
uk.140 ibara ya 191 ya Hotuba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji. Serikali imepanga kutekeleza mambo 9 na katika mambo yote
hayo hakuna hata moja linalohusiana na Viwanda vya kuzalisha bidhaa
zinazohudumiwa na wananchi wengi zaidi kama Sukari na Mafuta ya kula.
Bidhaa hizi ni bidhaa zinazoleta maneno ya kisiasa ndani ya nje ya
Bunge. Nadhani baada ya madawa ya kulevya, bidhaa zenye mizengwe mingi
zaidi katika duru za kisiasa ni Sukari na Mafuta ya kula. Sukari na
Mafuta ya kula imeangusha Mawaziri kadhaa hapa nchini katika kipindi cha
miaka 20 iliyopita. Hata hivyo Wizara ya Viwanda na Biashara haina
mkakati kabisa kushughulika na Bidhaa hizi licha ya uwezo wake wa
kutenegenza ajira na kuokoa fedha za kigeni kuziagiza. Wizara
imezungumza kuhusu viwanda vya nguo lakini haijafafanua changamoto kubwa
zinazoikabili sekta ya nguo nchini na hasusan biashara haramu ya
magendo ya Nguo inayoathiri sana ukuaji wa sekta ya nguo nchini.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ukitazama hotuba ya Waziri wa
Kilimo ambayo Bunge lako tukufu limeshapitisha bajeti yake kuna
‘mikakati’ ya kulima Miwa kwa ajili ya Sukari. Ukurasa wa 44 ibara ya
107 ya Hotuba ya Wizara ya Kilimo na ukurasa wa 25 ibara za 63 na 64
zinaeleza ‘mikakati’ ya kukabiliana na uhaba wa Sukari nchini.
Kiambatanisho namba 6 cha Hotuba hiyo kimeeleza kwa kina changamoto
nzima ya Sukari na miradi ianyopaswa kutekelezwa ili kumaliza kabisa
suala la uhaba wa Sukari nchini. Nimejumlisha miradi ile kutoka kona
mbalimbali za nchi na nimekuta ni takribani Hekta 300,000 za kulima
Miwa. Kwa Hesabu ya chini ya wastani wa kuzalisha Sukari kwa kila Hekta,
miradi hii ikitekelezwa Tanzania itaweza kuzalisha Tani 1.5 milioni za
Sukari. Ukiondoa Sukari tunayotumia nchini, ziada itakayouzwa nje
inaweza kuliingizia Taifa Fedha za Kigeni USD 500 milioni, sawa na 30%
ya malengo ya Mpango wa Maendeleo kwa sekta ya Viwanda katika mapato ya
Fedha za kigeni ya USD 3bn. Hapo sijaeleza kiwango cha Ajira
kitakachopatikana, ukuaji wa biashara kwenye sekta nyengine na Umeme
utakaozalishwa ( Multiplier effect ).
Mheshimiwa Spika, swali la kujiuliza, chukulia Wizara ya
Kilimo inalima hiyo miwa hekta 300,000 halafu Wizara ya Viwanda haina
mpango wa hivyo viwanda, hii miwa itakwenda wapi? Sio kwamba inapaswa
kufungaminisha Kilimo cha Miwa na Viwanda vya Sukari? Ni kwa nini Wizara
2 zilizo chini ya Serikali moja zinashindwa kusomana? Baraza la
Mawaziri linajadili nini? Ndio maana Rais anajikuta akitoa matamshi ya
Mawaziri barabarani. Suala la Rais kutoa matamko kuhusu Sukari sio sawa,
hii ni Kazi ya Mawaziri maana mnam expose Rais. Rais sio mtu wa
kuhangaika na masuala ya kunywa Chai na Uji.
Mheshimiwa Spika, nashauri Bunge lako tukufu leo
lisipitishe Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili
Wizara hii ikakae na Wizara ya Kilimo wawianishe mipango hii na kisha
walete hapa Bungeni ndio tupitishe.
0 comments:
Post a Comment